TAARIFA KWA UMMA JUU YA UWEPO WA BIDHAA YA MCHELE UNAODHANIWA KUTENGENEZWA KWA PLASTIKI

image

Hivi karibuni zimeibuka taarifa kupitia video na picha kupitia mitandao ya kijamii (“Instagram na WhatsApp”) zinazoelezea hofu ya uwepo wa bidhaa ya mchele inayosadikika kutengenezwa kutokana na plastiki. Baadhi ya video hizo zinaonesha mtambo unaosadikika kutengeneza mchele kutokana na mifuko ya plastiki, huku nyingine zinaonesha wali ukifinyangwa kisha kudundisha kwenye sakafu kama mpira.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likiwa na dhamana ya kulinda usalama na ubora wa bidhaa zinazotumika hapa nchini ikiwamo bidhaa ya mchele kwa Sheria ya Viwango Namba 2 ya mwaka 2009, baada ya kupata taarifa hizo lilifanya utafiti katika soko (surveillance) ambapo jumla ya sampuli 21 za aina mbalimbali za mchele zilichukuliwa katika maeneo mbalimbali ya masoko na kupimwa ubora wake katika maabara za TBS. Majibu ya uchunguzi wa maabara yanaonesha mchele uliopo katika soko la Tanzania ni salama kwa matumizi ya binadamu kwani unakidhi mahitaji ya kiwango cha Tanzania na cha Jumuiya ya Afrika Mashariki “TZS 592/EAS128, Milled rice — Specification”. Vilevile, sampuli zilizopimwa hazina kiambata chochote cha plastiki.
Kutokana na majibu hayo ya kisayansi, Shirika linapenda kuufahamisha umma kwamba, taarifa zinazosambaa kuhusiana na kadhia hii kimsingi hazina ukweli wowote.  Ni vema kufafanua kwamba mashine inayooneshwa kwenye video kuwa inatengeneza mchele wa plastiki ni mashine inayotumika katika utaratibu wa kawaida kwenye viwanda vya plastiki katika utengenezaji wa malighafi za plastiki “production, recycling of used plastic materials” katika mfumo wa punje ndogo ambazo zinaweza kutafsiriwa vibaya kwamba ni punje za mchele.
Vilevile Video nyingine inayoonesha kunata na kudunda kwa mchele uliopikwa, hii hutokea kwa bidhaa ambazo zina viambata vya wanga “starch” pale zinapopikwa huvutika “gelatization” ambapo nyingine hufikia hatua ya kudunda kama vile ugali wa muhogo na wa ngano. Hata hivyo kinachooneshwa katika video hizo hakina uhalisia kwamba ni mchele wa plastiki.
Kwa taarifa hii, Shirika linatoa rai kwa umma kutoa ushirikiano kwa yeyote ambaye anao mchele huo kutoa taarifa na kuleta sampuli TBS, ili ufanyiwe uchunguzi wa kitaalamu katika maabara za TBS zenye umahiri wa kimataifa “ISO 17025” badala ya kutia hofu wananchi kwa vitu visivyo na ukweli. 
Kwa kutoa taarifa hizo tafadhali piga simu (Hotline) ya bure namba 0800 110 827 kwa kutumia mtandao wa Vodacom na TTCL au kwa barua pepe .(JavaScript must be enabled to view this email address)

Kwa taarifa zaidi wasiliana na

Mkurugenzi Mkuu
Shirika la Viwango Tanzania
Morogoro/Sam Nujoma Roads, Ubungo
P.O. Box 9524 Dar es Salaam, Tanzania


Tafadhali bofya linki ifuatayo ili uweze kupakua taarifa hii:

Press_release_mchele_wa_plastic_3_tracked-1.pdf