TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAFUTA YA ALIZETI

Hivi karibuni imeripotiwa na watafiti wa kisayansi wa Michigan State University, Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na kuchapishwa katika jarida la PLoS ONE kuwa mbegu za alizeti zinazotumika kuzalisha mafuta ya alizeti na mashudu yake ambayo hutumika hapa nchini, zina kiwango kikubwa cha sumu kuvu inayosababisha kansa.

Hata hivyo, kiwango kikubwa cha sumu kuvu katika mbegu za alizeti na mashudu siyo kiashirio kuwa mafuta yatokanayo na mbegu hizo kuwa yatakuwa na kiwango hatarishi cha sumu kuvu hii ni kutokana na hatua zinazotumika katika uzalishaji wa mafuta ya alizeti yanayozingatia kiwango husika.

Shirika la Viwango Tanzania ni Shirika pekee hapa nchini lenye dhamana ya kuandaa viwango vya bidhaa mbalimbali ambalo lina jukumu la kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazotoka nje ya nchi zinakidhi matakwa ya viwango vya bidhaa husika kabla ya kuingia sokoni. Mafuta ya alizeti ni miongoni mwa bidhaa ambazo ziko katika orodha ya bidhaa ziliizo chini ya viwango vya lazima. Hivyo basi wazalishaji wote wa mafuta ya alizeti wanatakiwa kuzalisha kwa kuzingatia kiwango cha kitaifa TZS 50:2014 ambacho kimeoanishwa katika ngazi ya Afrika Mashariki, EAS 299:2013.

Kiwango cha mafuta ya alizeti cha Afrika Mashariki kinatumiwa na nchi zote wanachama katika kudhibiti ubora wa mafuta ya alizeti na hujumuisha upimaji wa sumu kuvu ambazo huathiri nafaka.

Kiwango cha Tanzania cha mbegu za alizeti TZS 1578:2012 na kiwango cha mashudu ya alizeti, TZS 819:2004   vinatoa muongozo kwa mzalishaji unaomwezesha kuzalisha mafuta bora na salama kwa mtumiaji na vilevile chakula bora na salama kwa wanyama.

Mafuta ya alizeti yaliyothibitishwa ubora wake na TBS huwekwa alama ya ubora ya ‘tbs’ hivyo kumwezesha mlaji kuitambua bidhaa yenye ubora sokoni na kufanya uchaguzi sahihi.

Kwa taarifa hii, TBS inawakumbusha wazalishaji wote wa mafuta ya alizeti kuhakikisha kuwa wakati wote bidhaa zao zinakidhi ubora na kuthibitisha ubora wa bidhaa kabla ya kuingiza sokoni. Wakati huohuo wauzaji wote wa mafuta ya alizeti wanaaswa kuhakikisha kuwa wanauza mafuta yenye alama ya ubora ya tbs.

ANGALIZO: Mtumiaji wa bidhaa hakikisha kuwa wakati wote unatumia bidhaa iliyothibitishwa ubora wake na TBS .

Limetolewa na:

Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Shirika la Viwango Tanzania,
S.L.P. 9524,
Dar Es Salaam,
Simu: +255(022) 2450206
Hotline:+0800110827
Barua pepe: .(JavaScript must be enabled to view this email address)
Website: http://www.tbs.go.tz

Tafadhali bonyeza linki ifuatayo ili uweze kupakua tangazo hili:

TAARIFA_KWA_UMMA_KUHUSU_MAFUTA_YA_ALIZETI.pdf