Chakula Salama Huimarisha Utoshelevu wa Chakula

Posted On: Oct, 20 2020
News Images

Chakula ni hitaji linalopewa kipaumbele kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu wake kwa maisha ya binadamu, uchumi na maendeleo. Kwa kuzingatia umuhimu huo, jitihada mbalimbali hufanyika ili kuwezesha uwepo wa uhakika wa chakula kinachotosheleza mahitaji (food security) pamoja na kuhakikisha kuwa chakula ni salama ili walaji wasipate madhara ya kiafya.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilianzisha “Siku ya Chakula Duniani” ambayo huadhimishwa tarehe 16 Oktoba kila mwaka ikiwa ni wito wa kuamsha ari ya uzalishaji wa chakula cha kutosheleza ili kutokomeza baa la njaa na lishe duni duniani. Mwaka huu wa 2020, siku hii inaadhimishwa kwa kuongozwa na kauli mbiu isemayo “Vitendo vyetu ni mustakabali wetu” ("Our actions are our future”).

Kwa mujibu wa FAO, uteshelevu wa chakula hufikiwa pale ambapo kila mtu na kwa wakati wote anapata chakula cha kutosha, ambacho ni salama na kinachokidhi mahitaji ya lishe mwilini. Hii inaonesha kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya suala la uteshelevu wa chakula na usalama wa chakula. Kwa mantiki hiyo, usalama wa chakula ni hitaji la msingi katika kukidhi azma ya utoshelevu wa chakula kutokana na ukweli kwamba hata kama chakula kinapatikana kwa wingi na cha kutosheleza, endapo hakitakuwa salama kinapomfikia mlaji, basi kinaweza kusababisha matokeo hasi kiafya, kibiashara na kiuchumi. Hivyo basi, suala la usalama wa chakula hutiliwa mkazo ili kuhakikisha upatikanaji wa manufaa yanayokusudiwa katika utoshelevu wa chakula. Chakula kinapokuwa salama huwezesha kulinda afya ya walaji, kupunguza gharama za matibabu, uhakika wa chakula, lishe bora, biashara ya chakula ndani na nje ya nchi, utalii, maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii n.k.

Umuhimu wa usalama wa chakula umeendelea kupewa kipaumbele kitaifa na hata kimataifa ambapo mnamo mwaka 2018, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (The United Nations General Assembly) lilipitisha azimio la kuadhimisha Siku ya Usalama wa Chakula Duniani (World Food Safety Day) kila ifikapo tarehe 7 Juni kuanzia mwaka 2019 kwa lengo la kuimarisha uelewa katika kufanikisha usalama wa chakula.

Kimsingi, “Chakula kinakuwa salama pale ambapo hakijachafuliwa na vimelea vya maradhi (phathogenic micro-organisms), kemikali za sumu (chemical contaminants) au takataka (physical contaminants) kwa kiwango kinachoweza kumsababishia mlaji madhara ya kiafya”

Vimelea vya maradhi kama vile bakteria, virusi na minyoo hupatikana katika udongo, maji, hewa, miili ya binadamu, wanyama n.k na huingia katika chakula endapo mbinu bora za usafi hazitazingatiwa katika hatua za uzalishaji, uvunaji, usafirishaji, usindikaji, uhifadhi au uandaaji wa chakula. Mambo yanayosababisha chakula kuchafuliwa na vimelea vya maradhi ni pamoja na uandaaji kufanyika katika mazingira ya uchafu, kutumia maji na vyombo visivyo salama, wasindikaji na waandaaji wa chakula kutozingatia kanuni bora za usafi na afya.

Uchafuzi wa kemikali kwenye chakula husababishwa na uwepo wa vihatarishi vifuatavyo:- Mabaki ya viuatifu (pesticide residues) vinavyotumika kuzuia au kuua wadudu kwenye mazao ya chakula wakati wa uzalishaji au uhifadhi; Mabaki ya dawa za kutibu mifugo (veterinary drug residues) kwenye bidhaa za chakula zitokanazo na wanyama kama vile nyama, mayai au maziwa kutokana na kutozingatiwa muda wa kusubiri (withdraw period) baada ya mnyama kutibibiwa na kabla ya kumchinja au kabla ya kutumia maziwa au mayai yake; Madini tembo (heavy metals) kama vile risasi (lead), zebaki (mercury) na cadmium ambayo huingia kwenye mazao ya chakula endapo kilimo, uvuvi na ufugaji vitafanyika katika mazingira ambayo udongo, maji au hewa vimechafuliwa na madini hayo; Sumukuvu (mycotoxon) zinazozalishwa na baadhi ya fangasi au kuvu kwenye mazao ya chakula hususan mahindi na karanga; Sumu asili (natural toxins) zinazokuwepo kwenye baadhi ya mazao ya chakula kama aina ya mihogo michungu na baadhi ya uyoga. Uchafuzi wa kemikali husababishwa pia na matumizi yasiyo sahihi ya vikolezo (food additives) wakati wa usindikaji wa chakula; Aidha, vihatarishi vingine vya usalama wa chakula ni vitu kama vile vipande vya mifupa, mawe, miti, chupa, chuma n.k ambapo vinapokuwa kwenye chakula huweza kusababisha majeraha au madhara kwenye meno, koo au kinywa cha mlaji.

Endapo chakula si salama, kinapoliwa kitamsababishia mlaji madhara ya kiafya ambayo yanaweza kutokea baada ya muda mfupi au hata baada ya muda mrefu kutegemea aina na kiasi cha vimelea au kemikali kinachoingia mwilini, umri wa mlaji, hali ya kiafya na kinga mwili kwa ujumla.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha kuwa takriban watu milioni 600 duniani kote sawa na mtu mmoja kati ya wati 10 huugua kila mwaka na kati yao, 420,000 hupoteza maisha kutokana na kula chakula kisicho salama. Kwa kuzingatia takwimu hizo pamoja na uwepo wa vihatarishi vinavyoweza kuathiri usalama wa chakula na ongezeko la utandawazi katika biashara ya chakula, ni muhimu kuendelea kutilia mkazo suala la kuhakikisha kuwa chakula chetu ni salama.

Mambo ya yanayopaswa kufanyika ili kuhakikisha usalama wa chakula ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya viuatiifu wakati wa kilimo na uhifadhi wa mazao. Viuatilifu visipotumika kwa usahihi husababisha mabaki yake (pesticide residues) kuwepo kwenye chakula na hivyo kuathiri usalama wa chakula husika. Vilevile, ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kutibu mifugo, kanuni bora za usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na uandaaji wa chakula. Aidha, ili kuepuka magonjwa yatokanayo na ulaji wa chakula kisicho salama, inapaswa kuzingatia usafi wakati wa kuandaa chakula ikiwa ni pamoja na usafi wa mtu anayeandaa na usafi wa mazingira ya kuandalia chakula; kuhakikisha kuwa chakula kilichopikwa kinatenganishwa na chakula kibichi ili kuepuka vimelea kutoka chakula kibichi visiingie kwenye chakula kilichopikwa.Hali kadhalika, ni muhimu kupika chakula mpaka kiive vizuri ili kuua vimelea vya maradhi, kuhifadhi chakula kilichopikwa kwa uangalifu ili kisichafuliwe na vimelea au kemikali na kutumia maji na malighafi safi salama katika uandaaji wa chakula.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na mambo mengine hutekeleza majukumu mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini ikiwa ni pamoja na kuandaa Viwango vya Chakula vya Kitaifa (National Food Standards) kwa kuzingatia misingi ya kisayansi. Viwango hivyo hutumika na kuzingatiwa katika uzalishaji au usindikaji wa chakula pamoja na udhibiti wa usalama na ubora wake. Majukumu mengine kufanya uchunguzi wa sampuli za chakula katika maabara, kufanya tathmini ya bidhaa na kuzisajili, kufanya ukaguzi katika soko pamoja na maeneo ya usindikaji, usafirishaji na uhifadhi na usambazi wa chakula, kudhibiti uingizaji nchini na usafirishaji wa chakula nje ya nchi opamoja na kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya usalama wa chakula.

Ni muhimu kutambua kuwa usalama wa chakula huweza kuathirika katika hatua mbalimbali za mnyororo wa chakula (food value chain) kuanzia mazao yanapokuwa shambani na wakati wa uvunaji, usafirirshaji, uhifadhi, usindikaji, uandaaji na ulaji. Kwa mantiki hiyo, ili kutimiza azma ya kuhakikisha uwepo wa chakula kilicho salama wakati wote, wadau wote katika mnyororo wa chakula ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, wavuvi, wasindikaji, wasafirishaji, wahifadhi, wafanyabiashara na walaji wa chakula wanapaswa kutekeleza kikamilifu wajibu wao katika kuhakikisha kuwa chakula hakichafuliwi na vimelea vya maradhi, kemikali za sumu au takataka. Aidha, Serikali kwa upande wake imekuwa ikiwajibika na kutoa kipaumbele katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kuweka sera, sheria, mifumo, rasilimali na miundombinu inayohitajika.