Chakula Bora na Salama ni Jukumu la Kila Mmoja katika Mnyororo wa Thamani

Posted On: Oct, 20 2020
News Images

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani huratibiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na kufanyika duniani kote tarehe 16 Oktoba kila mwaka. Maadhimisho ya mwaka huu 2020, yanafanyika wakati ambapo ulimwengu unashuhudia mafanikio makubwa katika kupambana na umaskini, njaa pamoja na ukosefu wa lishe ya jamii. Mafanikio haya yametokana pamoja na mambo mengine, kilimo cha mazao ya chakula, ikifungamana na mifumo madhubuti ya udhibiti wa ubora na usalama wa chakula duniani. Aidha, pamoja na mafanikio haya, takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonesha kuwa inakadiriwa watu zaidi ya bilioni mbili hukosa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho vinavyotosheleza katika mwili.

Ikumbukwe kuwa, chakula ni hitaji muhimu kwa maisha ya binadamu, ustawi na maendeleo ya nchi. Umuhimu huu unasababisha suala la ubora na usalama wa chakula kupewa kipaumbele katika kulinda afya ya jamii, kuwezesha uhakika wa chakula na lishe (food and nutrition security), kukuza uchumi na kuwa kigezo muhimu katika biashara ya chakula kitaifa na kimataifa. Vilevile, ubora na usalama wa chakula ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals), hasa malengo namba 1, 2 na 3 yahayohusu kuondoa umaskini, kutokomeza njaa pamoja na kulinda afya ya jamii na ustawi.

Pamoja na kukosa ushindani katika soko, chakula kisicho bora huweza kusababisha upotevu wa chakula (food loss). Kwa mujibu wa takwimu za FAO, asilimia 14 ya chakula kinachozalishwa duniani kila mwaka hupotea kabla ya kufikia soko la jumla. Vilevile, chakula kisicho bora huweza kusababisha madhara ya kiafya kama vile magonjwa na hata vifo. Takwimu za madhara ya kiafya zilizotolewa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) mwaka 2015 zinaonesha kuwa takriban watu milioni 600 duniani, ambayo ni sawa na mtu mmoja kati ya watu 10 huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao, 420,000 hupoteza maisha. Aidha, tatizo hili limedhihirika kuwa kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.

Pamoja na athari za kiafya, ni vema kufahamu pia kuwa, chakula kisichokuwa bora huzorotesha maendeleo na hivyo, uchumi katika ngazi zote na kusababisha athari za kijamii. Kwa mantiki hiyo, mfumo imara wa udhibiti wa ubora na usalama wa chakula ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuinua biashara ya mazao ya chakula na hivyo kukuza uchumi.

Mfumo madhubuti wa udhibiti ubora na usalama wa chakula ni ule wenye kukidhi misingi mikuu mitano, ikiwa ni pamoja na mfumo huo kujengwa katika msingi wa sheria, msingi thabiti wa ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara, msingi wa elimu kwa umma na mawasiliano.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hutekeleza majukumu yake chini ya Sheria ya Viwango, Sura 130. Katika kutekeleza majukumu haya, kazi ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula nchini ni mojawapo ya jukumu la kisheria na la msingi la TBS. Kwa kutambua na kuzingatia umuhimu wa ubora na usalama wa chakula, TBS imeweka mfumo thabiti ili kuhakikisha chakula kinachozalishwa ndani ya nchi na kile kinachoingizwa nchini kinakidhi vigezo vya usalama na ubora. Baadhi ya majukumu yanayotekelezwa na TBS katika kuhakikisha ubora na usalama wa chakula nchini ni pamoja na:-

i)Kuandaa viwango vya bidhaa za kilimo na chakula

ii)Kusajili maeneo na kutoa vibali vya biashara ya vyakula;

iii)Kufanya ukaguzi wa chakula katika soko pamoja na ukaguzi wa maeneo ya kusindikia, kuhifadhi na kuuzia chakula;

iv)Kudhibiti uingizaji nchini na usafirishaji wa vyakula nje ya nchi;

v)Kufanya uchunguzi wa bidhaa za chakula katika maabara;

vi)Kufanya ufuatiliaji wa usalama wa bidhaa za chakula katika soko;

vii)Kuelimisha jamii kuhusu masuala muhimu juu ya ubora na usalama wa chakula;

Aidha, suala la ubora na usalama wa chakula ni mtambuka, likihusisha wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja walaji, wakulima, wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara, n.k katika kuhakikisha ubora na usalama katika mnyororo wa thamami kuanzia mazao ya chakula yakiwa shambani hadi chakula kinapomfikia mlaji. Sekta ya habari ni mdau muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubora na usalama wa chakula.

‘‘Chakula bora na salama ni jukumu la kila mmoja katika mnyororo wa thamani’’ hivyo, kila mmoja atekeleze wajibu wake, mfano kuzingatia kikamilifu kanuni bora za kilimo, ufugaji, usindikaji na uandaaji na usambazaji katika hatua mbalimbali za mnyororo wa chakula.