Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kwa Ufupi

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 1975 na kuanza kazi rasmi tarehe 16 Aprili 1976, kisha kuundwa upya kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 2009 iliyoifuta sheria ya kwanza. Sheria mpya imelipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora.

Sheria mpya ya Viwango imebainisha hatua zifuatazo zitakazochukuliwa pindi inapobainika kuwepo kwa bidhaa hafifu:-

a) Kuondoa bidhaa hafifu zilizopo sokoni;
b) Kufuta leseni;
c) Kuweka utaratibu wa marejesho na/au fidia;
d) Kuweka taratibu za kuharibu bidhaa duni au kuzirudisha zilikoagizwa;
e) Kutoza faini.

Sheria hii imeambatana na kanuni nne za utekelezaji ambazo ni:

a) Kanuni za usimamizi wa alama ya ubora;
b) Kanuni za Ithibati ya Ubora (Certification Regulations);
c) Kanuni za Upimaji wa Bidhaa (Tested Products Regulations);
d) Kanuni za Idhibati ya Ubora wa Shehena (Compulsory Batch Certification Of Imports Regulations);


MAJUKUMU YA TBS
Kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009, TBS ina majukumu yafuatayo:

a) Kuweka, kurekebisha na kusimamia viwango vyote vya kitaifa;
b) Udhibiti wa ubora wa bidhaa za ndani na nje;
c) Kutoa ushauri viwandani juu ya uzalishaji wa bidhaa bora;
d) Kupima na kuhakiki vipimo vinavyotumika viwandani;
e) Kuelimisha umma juu ya masuala ya viwango;
f) Kutoa leseni za matumizi ya alama ya ubora kwa bidhaa za ndani na nje zilizokidhi viwango stahili.

Kwa ujumla, jukumu la jumla la Shirika ni kukuza matumizi ya viwango na kuinua ubora wa bidhaa na huduma nchini ili kupanua na kuimarisha soko la ndani na nje. 

DIRA YETU

Sanjari na Malengo ya Maendeleo ya Milenia, Dira ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuelekea mwaka 2015 ni kuwa taasisi inayotambulika kitaifa na kimataifa kama kitovu cha umahiri na weledi katika ukuzaji wa viwango na udhibiti wa ubora. TBS imedhamiria kufanikisha yafuatayo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015:

a) Kuwa na mfumo wa usimamizi wa ubora unaofanya kazi kwa kuzingatia Kiwango cha ISO 9001;

b) Kuhakikisha kuwa Kitengo cha Ukaguzi kinapata cheti cha umahiri kwa kuzingatia matakwa ya Kiwango cha ISO 17020;

c) Kuhakikisha kuwa Kitengo cha Ithibati ya Ubora wa Bidhaa kinapata cheti cha umahiri kwa kuzingatia matakwa ya Kiwango cha ISO 17065;

d) Kuhakikisha kuwa Kitengo cha Ithibati ya Mifumo ya Ubora kinapata cheti cha umahiri kwa kuzingatia matakwa ya Kiwango cha ISO 17021;

e) Kuhakikisha kuwa maabara zote zinapata vyeti vya umahiri kwa kuzingatia matakwa ya Kiwango cha ISO 17025;

f) Huduma kwa wateja zinatolewa kwa ufanisi zaidi kwa kutumia teknolojia ya kisasa;

g) Ofisi za kanda zinaanzishwa Mwanza, Mbeya na Arusha;

h) Wajasiriamali wadogo wapatao 300 wanapata leseni za kutumia alama ya ubora ya TBS kwenye bidhaa zao;

i) Mfumo wa ithibati ya ubora wa huduma unatekelezwa na kuhakikisha kuwa takriban kampuni 20 zinapata vyeti vya ubora chini ya mfumo huu;

j) Takriban kampuni 40 zinapewa mafunzo na kupata ithibati ya ubora wa mifumo yao kwa kuzingatia viwango vya ISO 9000, ISO 14000, ISO 22000 (vya usimamizi wa ubora) na OHSAS 18000 (cha usimamizi wa usalama katika maeneo ya kazi); na

k) Kuhakikisha kuwa wafanyakazi wake wanapewa mafunzo muafaka na kulindwa wao na familia zao dhidi ya magonjwa na sulubu, ili waweze kuwa na tija zaidi.

DHIMA YETU

Dhima ya Shirika la Viwango Tanzania ni kueneza uelewa na kukuza matumizi ya viwango na kanuni za udhibiti wa ubora katika sekta za viwanda na biashara, kwa nia ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuzalisha bidhaa na huduma bora zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje, lengo likiwa ni kukuza uwepo wa bidhaa na huduma bora na salama kwa umma wa Watanzania na kuchochea maendeleo ya Taifa kiuchumi.

SERA YETU YA UBORA

Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa kuzingatia dhamana liliyopewa, linahakikisha kutoa huduma bora, ambazo ni pamoja na utayarishaji wa viwango na uhakiki wa ubora, kwa kukidhi na hata kuvuka matakwa ya wateja, ili kudumisha imani yao. TBS hutoa rasilimali na kuboresha mifumo ya utendaji wake mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba wafanyakazi wake wanakuwa na uwezo wa kutoa kwa wakati huduma bora wakati wote na kwamba kila mfanyakazi anawajibika kwa ubora wa kazi yake.

OFISI ZA TBS
Licha ya ofisi za Ubungo, Dar es Salaam, Shirika lina ofisi katika mipaka ya Sirari, Holili, Horohoro, Bandari ya Tanga na Namanga.  Shirika hutekeleza majukumu yake mbalimbali katika mipaka iliyobaki kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka mbalimbali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Mazingira (NEMC), Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

UANACHAMA
Katika kulinda maslahi ya nchi kiuchumi na kibiashara, Shirika ni mwanachama na hujihusisha kikamilifu na shughuli za mashirika ya viwango ya kimataifa yafuatayo:

a) Shirika la Viwango la Kimataifa (International Organization for Standardization, ISO);
b) FAO/WHO Codex Alimentarius Commission;
c) Shirika la Viwango Kanda ya Afrika (African Regional Organization for Standardization, ARSO);
d) SADC Expert Group on Standardization, Quality Assurance, Metrology and Testing (SQMT);
e) Jumuia ya Afrika Mashariki (East African Community Committee for Standardization, Quality Assurance, Metrology and Testing).

UPIMAJI WA UBORA WA BIDHAA TBS
Upimaji wa ubora wa bidhaa huhusisha:

a) Mazingira ya uzalishaji, mazingira yanayotakiwa ni yale yaliyopitishwa na bwana afya na kuhakikiwa na mkaguzi wa TBS;
b) Bidhaa husika ili bidhaa ipite ubora mzalishaji anashauriwa afuate malekezo ya uzalishaji yaliyoainishwa ndani ya kiwango cha bidhaa husika kipatikanacho TBS;
c) Kifungasjio ni lazime kiwe kile kilichokusudiwa kwa bidhaa husika;
d) Lebo inatakiwa iwe na maelezo sahihi juu ya bidhaa husika;
e) Bidhaa za kutoka nje ya nchi hupimwa ndani ya nchi zinapotoka au sampuli huchukuliwa bandarini (Tanzania) na kupimwa kabla ya kuingia ndani ya nchi. Bidhaa hafifu haziruhusiwi kuingia nchini.

MAABARA ZA TBS
TBS ina maabara tisa zenye vifaa vya kisasa na wataalamu wa kutosha. Maabara hizo ni kama ifuatavyo:

a) Maabara ya kemia – Maabara hii inapima kemikali, petroli na bidhaa zake na madini yaliyomo katika bidhaa mbalimbali kama sabuni, dawa za mbu, maji, soda, bia n.k.

b) Maabara ya Chakula – Maabara hii inapima ubora wa vyakula na bidhaa za kilimo. Maabara hii ina sehemu mbili: Upande wa kemikali na upende wa vijiumbe. Kiasi cha kemikali, wadudu, asidi, vitamini, unyevu, mafuta n.k kwenye bidhaa huweza kutambuliwa kupitia maabara hii.

c) Maabara ya uhandisi mitambo – Mitambo mbalimbali hupimwa katika maabara hii, kwa mfano ubora wa bidhaa kama nondo hupimwa hapa na kujua ugumu au ulaini wake, ustahimilivu na kuvunjika kwake, na hata urefu na upana wake na kama inafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa.

d) Maabara ya uhandisi umeme – Maabara hii hupima ubora wa bidhaa za umeme kama vile nyaya, swichi, taa, soketi n.k.  Vifaa hivi huangaliwa kama viko kwenye ubora unaotakiwa ili visije vikaleta madhara kama moto.

e) Maabara ya uhandisi ujenzi – Maabra hii ina uwezo wa kupima bidhaa zinazotumika kwenye ujenzi kama vile matofali, mchanga, vigae, saruji, mbao, n.k. Pia maabara hii una uwezo wa kupima ujenzi uliokamilika kama umefuata matakwa ya viwango au la.

f) Maabara ya ngozi, nguo na kondomu – Hapa kondomu, ngozi za viatu, soli, na ubora wa nguo hupimwa. Kwa mfano kwa upande wa nguo maabara hii huweza kubaini kama inachuja, inakunjikakunjika, uzito wake, kama ni pamba halisi au nailoni n.k. Pia hupima kondomu na kuzithibitisha kama zinafaa kwa matumizi.

g) Maabara ya ugezi – Maabara hii ni nyumbani kwa sayansi ya vipimo. Vipimo vitumikavyo kupimia vitu kama mizani, vipimajoto na mita mbalimbali huweza kurekebishwa ili kwenda sanjari na viwango vya vipimo. Pia matanki ya kuhifadhia mafuta na bidhaa nyingine hugeziwa hapa sanjari na viwango husika vya ujazo.

h) Kituo cha ufungashaji – Vifungashio vya bidhaa hupimwa ili kujua uwezo wao wa kuhimili misukosuko mbalimbali, ikiwamo ile ya usafirishaji.

i) Maabara ya pamba – Ubora wa pamba hupimwa katika maabara hii ili kukidhi kiwango cha kitaifa na kimataifa.

UTAYARISHAJI WA VIWANGO
Kama ilivyoainishwa hapo juu, moja ya kazi kubwa za Shirika la Viwango Tanzania ni utayarishaji wa viwango vya kitaifa.  Viwango hivi hutayarishwa na Kamati za Kitaalamu (