Je, Kiwango ni nini na vinatayarishwaje
Kiwango ni seti ya fasiri za kiufundi na miongozo, maelekezo ya “jinsi ya kufanya” kwa lengo la kuhimiza usalama, kutumainiwa, tija na ufanisi katika takribani kila tasnia. Viwango bi nyenzo ya mawasiliano kwa wazalishaji na watumiaji. Vinatumika kama lugha ya wote kuelezea ubora na kuweka vigezo vya usalama. Huandikwa na mabingwa wenye maarifa na utaalamu katika uwanja mahususi na wanaohudhuria kamati mbalimbali za ufundi.
Viwango hutayarishwa kwa kuziweka pamoja pande zote zinazohusika kama vile watengenezaji, walaji, na wadhibiti wa malighafi inayohusika, bidhaa, mchakato au huduma. TBS inakurugenzi iliyopewa wajibu na mamlaka ya kutunga viwango. Katika kurugenzi hii kuna zaidi ya kamati 100 za kiufundi. Viwango vingi vinatayarishwa kwa maombi ya tasnia husika. Hata hivyo, maombi yanaweza kutoka kwa watu binafsi, kamati, taasisi za kitaaluma, wakala za Serikali, vikundi vya tasnia, vikundi vya jamii au kutoka kwa kitengo au sehemu ya TBS. Maombi kwanza yanpelekwa kwenye kurugenzi inayohusika kwa ajili ya kufikiriwa. Baadaye kurugenzi hiyo hupangia kamati ya kiufundi inayohusika au huamua iwapo kamati mpya itahitajika. Kamati inayohusika ikishahitimisha kuwa kuna umuhimu wa kutosha na hufaa, mchakato wa kutayarisha kiwango kipya huanzishwa.