Tathmini ya vihatarishi katika chakula inahusisha tathmini ya hatari zinazohusiana na chakula au viambata vya chakula na tathmini ya hatari inayoweza kutokea kwa jamii ili kutoa ushahidi wa kisayansi ambao utasaidia kuweka hatua zinazofaa za udhibiti wa vihatarishi na kuandaa ujumbe sahihi kwa ajili ya mawasiliano kuhusiana na vihatarishi ili kuhakikisha usalama wa chakula na kulinda afya ya jamii. Kwa hiyo, tathmini ya vihatarishi katika chakula ni msingi wa kisayansi na sehemu muhimu na yenye ufanisi katika udhibiti wa usalama wa chakula katika Shirika.
Majukumu mahususi yanayofanyika ni pamoja na:
i) Kufanya ufuatiliaji wa hatari zitokanazo na kemikali, vimelea vya magonjwa na takataka kama vile vipande vya chuma na mifupa katika vyakula (visivyofungashwa na vilivyofungashwa), zinazoweza kusababisha madhara kwa mlaji;
ii) Kufanya tathmini ya hali ya ulaji wa chakula chenye uchafuzina kubainisha uwezekano na ukubwa wa madhara yanayoweza kutokea kwa mlaji;
iii) Kushauri juu ya masuala yanayohusiana na udhibiti wa vihatarishi katika chakula ili kuhakikisha usalama na kulinda afya ya jamii;
iv) Ufuatiliaji wa magonjwa yatokanayo na chakula;
v) Kujenga uelewa wa jamii juu ya vihatarishi vya usalama wa chakula na hatua za kupunguza vihatarishi hivyo; na
vi) Kuandaa, kuhuisha na kufanya mapitio ya taratibu na miongozo inayotumika katika tathmini ya vihatarishi vya chakula.