Uandaaji Viwango

Kiwango cha Tanzania ni Waraka ulioanzishwa kwa makubaliano na kuthibitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, unatoka na matumizi ya pamoja na wakati wote ya kanuni, miongozo au sifa bainifu za bidhaa na huduma na mifumo inayohusika au njia za uzalishaji, kwa lengo la kufikia kiwango cha juu cha ufuatiliaji sheria, kanuni na taratibu katika mahali husika. Pia inaweza kujumuisha au kushughulikia kipekee mahitaji ya istilahi/ msamiati, alama, ufungashaji, uwekaji alama kama yanavyotumika kwenye bidhaa, mchakato, usindikaji au njia ya uzalishaji. Kwa hiyo viwango vinasaidia kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma zinakidhi makusudio, kulinganisha na kulingana.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni Taasisi ya kisheria ya viwango vya kitaifa kwa Tanzania, iliyopewa wajibu na mamlaka ya kuandaa, kutangaza na kutekeleza viwango vya kitaifa. Kazi ya kuandaa viwango vya kitaifa inafanywa kupitia Kamati za Ufundi/ Kitaalamu za taifa zinazoratibiwa pekee na TBS.

Shirika lina mfumo wa uandaaji viwango wa taifa uliowekwa unaowezesha viwango vya kitaifa kuandaliwa. Mfumo huu unaofuata “Kanuni ya Makubaliano” inayofanya kazi kwa kutumia Kamati za Kiufundi/Kitaalamu. Kamati hizi huwa na wajumbe kutoka kwenye makundi ya wadau yakiwemo viwanda, Wizara na taasisi, taasisi za utafiti, taasisi za elimu, mashirika ya biashara na walaji.

Viwango vilivyokamilika ni pamoja na viwango vya bidhaa, viwango vya mfumo wa usimamizi, njia za upimaji, Kanuni za utendaji na kanuni za usafi. Viwango hivyo vinahusu sekta mbalimbali za uchumi, zikiwemo chakula na kilimo, kemikali na vifaa vya kitabibu, nguo na ngozi, ufundi umeme, umakanika na uhandisi wa metalajia, uhandisi ujenzi na ujengaji, mazingira, machimbo na madini na viwango vya jumla.

Viwango vinavyoandaliwa ni vya hiari, hata hivyo kama kiwango kinahusu bidhaa inayoweza kuathiri afya, usalama, mazingira au kinaweza kuleta athari kubwa kwa uchumi wa taifa, kiwango hicho kitachapishwa kama kiwango cha lazima.


Mchakato wa Uandaaji Viwango

Mdau yeyote, shirika la walaji, viwanda, vyama vya viwanda, taasisi za kitaalamu, wanachama wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na wajumbe wa Kamati za Kiufundi/Kitaalamu wanaweza kuwasilisha mapendekezo kwa TBS kwa ajili ya kuanzisha kiwango au kupitia upya, kurekebisha, au kubatilisha kiwango kilichokuwapo kwa kutuma maombi kwa maandishi.

Kazi ya uandaaji wa viwango kuhusu eneo lolote mahususi itafanywa wakati kamati ya kitengo husika itakaporidhika baada ya kupitia kwa makini au uchunguzi na ushirikiano na wanaohitaji kwamba umuhimu wa uandaaji viwango umeonekana.

Baada ya eneo husika kuchunguzwa na umuhimu wake kuonekana, kamati ya kitengo husika nayo itaipa jukumu la kutunga kiwango Kamati ya Kitaalamu/ Kiufundi inayohusika au Mkurugenzi Mkuu, atateua kamati ya Kitaalamu/ Kiufundi kwa madhumuni hayo.

Iwapo ombi la kuandaa kiwango kwa ajili ya eneo mahususi limekataliwa baada ya kuzingatiwa kwa makini, mpendekezaji wa ombi hilo ataarifiwa kuhusu uamuzi huo.

Rasimu ya kiwango iliyotayarishwa na kuthibitishwa na kamati itatolewa katika hali ya rasimu na kusambazwa sehemu mbalimbali kwa kipindi kisichopungua miezi miwili (Siku 60) miongoni mwa wenye mwelekeo mmoja kwa ajili ya kupitia kwa makini na kutoa maoni ya kuiboresha rasimu hiyo. Usambazaji sehemu mbalimbali unaweza kuachwa kama itaamuliwa hivyo na kamati ya kisekta kutokana na jambo hilo kuwa ni muhimu la haraka au halina utata.

Uzingativu mkubwa unatolewa kwenye maeneo ya fani mbalimbali, kama vile uhifadhi wa nishati, utunzaji wa mazingira, maendeleo ya vijijini na usalama.

Kwa hiyo, Kamati ya Ufundi/ Kitaalamu inayohusika, itakamilisha rasimu ya kiwango, kwa kuzingatia maoni yatakayopokelewa. Baada ya kuidhinishwa na kamati mahususi, rasimu ya kiwango inawasilishwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS kuidhinishwa kuwa Kiwango cha Tanzania kwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali na Waziri wa Viwanda na Biashara.

Viwango vyote vilivyoandaliwa hupitiwa upya kila baada ya muda, angalau mara moja kwa kila baada ya miaka mitano, kubaini haja ya kupitia upya kuvirekebisha au kuviondoa. Viwango ambavyo kwa maoni ya Kamati ya Kisekta havihitaji kupitiwa upya au kurekebishwa vinathibitishwa tena na Kamati ya Kiufundi/Kitaalamu.