SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA(TBS)
e-Services

Geita: Ubora wa bidhaa ni silaha ya ushindani – RAS

Reason Image

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Ndg. Mohamed Gombati, amewataka wazalishaji wa bidhaa mbalimbali katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera kuhakikisha bidhaa zao zinathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kupata alama ya ubora, kuimarisha uaminifu wa walaji na kupanua wigo wa masoko ndani na nje ya nchi.

Ndg. Gombati ametoa wito huo Oktoba 23, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya utoaji wa leseni za ubora kwa wazalishaji waliokidhi matakwa ya viwango vya kitaifa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi, iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Amesema kuwa uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango ni nyenzo muhimu ya kuongeza ushindani katika soko, kujenga imani kwa watumiaji na kuwawezesha wazalishaji kunufaika na fursa za kibiashara zilizopo katika masoko mbalimbali, ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuzingatia matakwa na taratibu zinazotumika katika masoko hayo.

“Ubora wa bidhaa ni silaha ya ushindani. Wazalishaji wanapaswa kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi matakwa ya viwango ili ziweze kuaminika na watumiaji na kuwapa fursa ya kushindana katika masoko yenye ushindani mkubwa,” amesisitiza.

Aidha, amewapongeza wazalishaji wadogo, wa kati na wakubwa waliokabidhiwa leseni za ubora kwa juhudi zao za kuwekeza muda, rasilimali na kuzingatia nidhamu ya uzalishaji ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ni bora na salama kwa watumiaji.

Amewahimiza wazalishaji hao kuitumia alama ya ubora ya TBS kama nyenzo ya kuongeza thamani ya bidhaa zao, kuimarisha ushindani na kutumia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.

Sambamba na hilo, Katibu Tawala huyo amewaagiza wataalamu wa TBS kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango, ili kuongeza uelewa wa wazalishaji na kuwajengea walaji uwezo wa kutambua na kudai bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango.

Pia, ameitaka TBS kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wateja, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, ambao ni miongoni mwa wadau muhimu katika kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa Magharibi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania, Dkt. Ashura Katunzi, amesema kuwa jumla ya wazalishaji 82 kutoka mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera wamekidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na kustahili kupewa leseni za ubora za TBS.

Amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Shirika za kuwawezesha wazalishaji kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango, kuimarisha usalama wa bidhaa sokoni na kuongeza imani ya watumiaji kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Hafla hiyo pia imeambatana na uzinduzi rasmi wa Ofisi ya TBS Kanda ya Ziwa Magharibi, yenye makao yake katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Ofisi hiyo inalenga kusogeza huduma za viwango karibu zaidi na wazalishaji na wadau wengine katika eneo hilo.

Utoaji wa leseni hizo pamoja na uzinduzi wa ofisi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya TBS na wazalishaji, kuongeza uelewa kuhusu viwango na kuchochea uzalishaji wa bidhaa bora na salama zinazoweza kushindana katika masoko mbalimbali.



Settings