Aina za Vifungashio Vinavyopimwa
Kituo kina uwezo wa kupima aina mbalimbali za vifungashio, zikiwemo:
-
Vifuniko na vizibo: Kama vile vifuniko vya chupa na makopo.
-
Vyombo vya kufungashia: Kama vile chupa, masanduku na makopo.
-
Lebo na alama: Kwa ajili ya utambulisho wa bidhaa na utoaji wa taarifa muhimu.
-
Vifaa saidizi vya ufungashaji: Vifaa vinavyosaidia kulinda, kufunga au kuimarisha vifungashio.
Malighafi za Vifungashio Vinavyopimwa
PTC ina uwezo wa kupima vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi zifuatazo:
-
Plastiki
-
Karatasi na ubao wa karatasi
-
Metali
-
Mbao
-
Nyuzi za nguo
-
Kioo
-
Malighafi mchanganyiko zenye tabaka mbalimbali
-
Mpira
Ithibati na Mipango ya Maendeleo ya Kituo
Kwa sasa, PTC imeidhinishwa kufanya upimaji wa vifungashio vilivyotengenezwa kwa karatasi na ubao wa karatasi. Kituo pia kinaendelea kuimarisha uwezo wake wa kupima vifungashio kamili na kutathmini usanifu wake.
Mipango ya maendeleo inajumuisha kutoa huduma za usanifu wa vifungashio vyenye ubora na kufanya tafiti kuhusu:
-
Muda wa bidhaa kukaa salama na bora (Shelf Life): Kutathmini muda ambao bidhaa inaweza kuhifadhi ubora wake inapowekwa kwenye kifungashio husika.
-
Uhamaji wa kemikali (Migration): Kuchunguza uwezekano wa kemikali kutoka kwenye kifungashio kuingia kwenye bidhaa, hasa vyakula.
-
Kiwango cha upitishaji wa vitu (Transmission Rates): Kutathmini kiwango ambacho vitu kama hewa, unyevunyevu na gesi hupita kupitia malighafi za vifungashio.
Umuhimu wa PTC kwa Viwanda na Watumiaji
Kituo cha Teknolojia ya Ufungashaji huchangia kuboresha ubora wa bidhaa, kulinda afya na usalama wa watumiaji na kuongeza ushindani wa biashara. Kupitia huduma zake, wazalishaji hupata mwongozo wa kuchagua vifungashio vinavyofaa, kuzingatia viwango husika, kupunguza upotevu wa bidhaa na kuongeza fursa za kuingia katika masoko ya ndani na nje ya nchi.