Tanzania yajitosheleza kwa chakula,yaimarisha ubora wa mazao
TANZANIA imepiga hatua katika uzalishaji wa chakula, hususan mazao ya nafaka, hali inayoiwezesha kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani na kuwa na uwezo wa kuuza ziada katika masoko ya nje.
Hatua hiyo inaashiria fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima, wafanyabiashara na taifa kwa ujumla, huku ikiweka umuhimu mkubwa katika kuimarisha ubora wa mazao ili kukidhi viwango vya ushindani wa kimataifa.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Robert Ngwasi, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 45 wa Kamati ya Kimataifa ya Wadau wa Viwango inayoshughulikia mazao ya jamii ya kunde na nafaka kwa ujumla.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wa viwango kutoka nchi 70 duniani kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu viwango vya ubora wa mazao hayo.
Ngwasi alisema Tanzania imeendelea kuimarisha uwezo wake katika uzalishaji wa chakula, hatua inayofungua fursa za kupanua biashara ya mazao ya kilimo nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanahitaji kuendana na uzalishaji wa mazao yenye ubora unaokubalika katika masoko mbalimbali ili wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo.
Alisema maandalizi ya viwango ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara kwa kuwa yanasaidia kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanakidhi matakwa ya soko, huku yakiongeza uwezo wa bidhaa za Tanzania kushindana na zinazozalishwa katika nchi nyingine.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo la uandaaji wa viwango na kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao yanayofaa na yanayoweza kuhimili ushindani katika soko huria,” alisema Ngwasi.
Alieleza kuwa ubora wa mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini umechangia kuijengea Tanzania heshima katika biashara, si katika mazao ya chakula pekee, bali pia katika bidhaa nyingine zinazozalishwa hapa nchini.
Alisema kuendelea kuimarisha viwango ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuimarisha zaidi nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.
Aidha, Ngwasi alisema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika.
Alisema fursa hiyo ni muhimu kwa nchi kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu viwango, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu zinazoweza kusaidia kuimarisha ubora wa mazao yanayozalishwa na kuuzwa katika masoko mbalimbali.
Ushiriki wa wajumbe kutoka nchi 70 duniani unaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuweka na kuboresha viwango vinavyotumika katika biashara ya mazao ya kilimo.
Kwa Tanzania, mkutano huo unatoa nafasi ya kuonesha uwezo wake wa uzalishaji na kujadiliana na wadau wengine kuhusu namna bora ya kuhakikisha bidhaa zake zinakidhi matakwa ya masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Candida Shirima, alisema katika kuandaa viwango, shirika hilo huzingatia matakwa na mahitaji ya wadau katika ngazi mbalimbali, yakiwemo ya kikanda, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), bara la Afrika na viwango vya kimataifa vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO).