Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara atembelea TBS Namanga
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma katika mpaka wa Namanga, akisema hatua hiyo imepunguza muda wa wafanyabiashara kufanya shughuli zao na kuongeza ufanisi wa biashara.
Londo amesema hayo wakati wa ziara ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika mpaka wa Namanga, iliyolenga kutembelea na kusikiliza maoni ya wafanyabiashara na wazalishaji kuhusu shughuli za biashara zinazoendelea katika mpaka huo.
Amesema ziara hiyo ni mwendelezo wa kawaida wa Wizara kutembelea wadau wake, wakiwamo wafanyabiashara na wazalishaji, kwa lengo la kuona namna shughuli zao zinavyotekelezwa na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Kwa mujibu wa Londo, mpaka wa Namanga ni miongoni mwa mipaka muhimu nchini kwa kuwa ni kituo kinachowezesha kuingizwa na kusafirishwa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini kwenda katika soko la Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.
Amesema Wizara pia ilipata fursa ya kutembelea shughuli zinazofanywa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambalo ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika mpaka huo.
“Kwetu sisi ni muhimu kuona ufanisi wa kazi zao kwa kiasi gani wanahudumia wafanyabiashara katika kuingiza, kuagiza na kusafirisha bidhaa katika mpaka wa Namanga,” amesema.
Londo amesema Wizara imefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya TBS na zaidi ya taasisi 18 za Serikali zinazofanya kazi katika mpaka huo, akieleza kuwa hali hiyo imekuwa na mchango katika kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wafanyabiashara.
Aidha, amesema Wizara ilipata fursa ya kusikiliza maoni ya watumiaji wa huduma ambao ni sekta binafsi, ambao alisema ndio walengwa wakuu wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Amesema wafanyabiashara hao wamefurahia hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuwajali na kupunguza muda wanaotumia kufanya shughuli zao za biashara ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
Londo amesema maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara yamechukuliwa na Wizara na yatafanyiwa kazi kwa pamoja ili kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.