Majukumu ya ukaguzi na utekelezaji wa sheria kwa ufupi
Kupitia Kitengo cha Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hufanya ukaguzi wa ufuatiliaji wa bidhaa katika soko na kufanya kaguzi maalum kwa lengo la kubaini, kuzuia na kuondoa bidhaa zisizokidhi matakwa ya Viwango, Kanuni na Sheria ya Viwango Sura 130. Shirika hutekeleza majukumu hayo katika masoko ya kawaida, viwanda vya uzalishaji, pamoja na majukwaa ya kidijitali na biashara za kielektroniki. Aidha, TBS hufanya vikao vya kimkakati na wadau kuhusu uzingatiaji wa matakwa ya viwango na kanuni, huhamasisha ushiriki wa umma katika kutoa taarifa kuhusu bidhaa zisizokidhi matakwa husika, pamoja na vitendo visivyo halali vinavyohusiana na ubora na usalama wa bidhaa.
Shughuli hizi za Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria hufanyika kwa mujibu wa vifungu vya 4(1)(a), (f), (j), (k) na (l), 4(2) na 20(6) vya Sheria ya Viwango, Sura ya 130 (Standards Act Cap 130). Lengo likiwa ni kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa na huduma ili kulinda afya ya jamii, mazingira na ustawi wa walaji.
Shughuli za ukaguzi na ufuatiliaji wa mwenendo wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko hufanyika kwa kuzingatia matakwa ya Kiwango cha Kimataifa cha ISO/IEC 17020, kinachosimamia shughuli za ukaguzi; ambacho TBS imepata ithibati yake. Ithibati hii inaonesha kuwa, TBS inakidhi matakwa yanayotambulika kimataifa katika umahiri wa kitaalamu katika kutekeleza majukumu ya ukaguzi na kutoa uhakika wa uwazi, uwajibikaji na kutopendelea upande wowote katika kutekeleza majukumu yake kama Taasisi ya Ukaguzi. Aidha, ithibati hiyo huongeza imani ya wadau kwa bidhaa na huduma katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Shughuli Mahususi za Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria
Shughuli zinazotekelezwa chini ya Kitengo cha Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria ni pamoja na:
- Kufanya ukaguzi wa ufuatiliaji wa bidhaa katika soko na viwandani;
- Kuchukua sampuli za bidhaa kwa kuzingatia tathmini ya vihatarishi kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara kwa lengo la kuhakiki ukidhi wa matakwa ya Viwango;
- Kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Viwango, pamoja na kuchukua hatua stahiki za kiudhibiti pale inapobidi;
- Kuzuia bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango pamoja na kusimamia urejeshwaji na uteketezaji wake kwa mujibu wa Sheria;
- Kutafsiri na kusambaza matokeo ya uchunguzi wa kimaabara yanayohusiana na ufuatiliaji usalama na ubora wa bidhaa zilizopo katika soko;
- Kufuatilia uzingatiaji wa miongozo kuhusu uhamasishaji na matangazo ya vyakula na vipodozi;
- Kuandaa, kusasisha na kupitia taratibu na miongozo ya kiutendaji inayotumika katika shughuli za ukaguzi na utekelezaji wa Sheria;
- Kutoa ushauri kuhusu hatua za kiutendaji zinazopaswa kuchukuliwa na Ofisi ili kuimarisha uzingatiaji wa viwango na matakwa ya kisheria.