Maabara za TBS zilianzishwa mwaka 1982 kwa lengo la:
(a)Kuwasaidia watengenezaji bidhaa kuongeza au kuimarisha ubora wa bidhaa zao
(b) Kutoka nyenzo za kupimia bidhaa kuhakikisha kufaa kwao kwa matumizi yaliyokusudiwa na;
(c) Kuhakikisha ubora wa bidhaa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi au kuingizwa nchini.
Maabara hizi pia zinatoa nyenzo za kupimia za haraka, sahihi na za siri kwa upimaji wa aina, upimaji wa uhakiki, ushauri wa kiufundi na maelekezo kuhusu mbinu za upimaji na mafunzo ya watumishi wa maabara.
1. Maabara ya Uhandisi Umeme
Maabara hii hupima ubora wa bidhaa za umeme kama vile nyaya, swichi, taa, soketi na vingine kadha wa kadha. Vifaa hivi huangaliwa kama viko kwenye ubora unaotakiwa ili visije vikaleta madhara kwa watumiaji.
2. Maabara ya Kemia
Maabara hii ilianzishwa ili kutoa huduma za upimaji wa bidhaa za kemikali na zile zenye muuanganiko wa kemikali.Mfano wa bidhaa zinazopimwa katika maabara hii ni sabuni zote kwa aina zake, viuatilifu, maji, petroli na bidhaa nyingine mbalimbali.
3. Maabara ya Uhandisi Ujenzi
Maabara hii ina uwezo wa kupima bidhaa zinazotumika kwenye ujenzi kama vile matofali, mchanga, vigae, saruji, mbao, n.k. Pia maabara hii ina uwezo wa kupima ujenzi uliokamilika kama umefuata matakwa ya viwango au la.
4. Maabara ya Pamba, Nguo na Ngozi
Hapa pamba, ngozi, nyavu, soli, nguo na bidhaa nyingine nyingi hupimwa. Kwa mfano kwa upande wa nguo, maabara hii huweza kubaini kama inachuja, inakunjikakunjika, uzito wake, kama ni pamba halisi na kadhalika.
5. Maabara ya Kemia ya Chakula
Maabara hii hupima ubora wa vyakula na bidhaa za kilimo.Maabara hii inapima kiasi cha kemikali, asidi, vitamini, unyevu, mafuta na maada nyingine kwenye bidhaa huweza kutambuliwa kupitia maabara hii.
6. Maabara ya Uhandisi Mitambo
Maabara hii hupima ubora wa mitambo na zana mbalimbali kama vile nondo, bati, pikipiki na vifaa na mashine mbalimbali ili kuangalia uimara, ustahimilivu na iwapo zana husika zinafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa.
7.Maabara ya Mikrobiolojia
Maabara hii hupima kiasi cha vijiumbe kinachopatikana katika bidhaa mbalimbali.
8. Kituo cha Teknolojia ya Ufungashaji
Ufungashaji ni sehemu muhimu sana katika biashara. Katika ulimwengu wa viwango, bidhaa isiyofungashwa vizuri hukosa ubora.
Ufungashaji si tu unatakiwa kutofautisha bidhaa moja na nyingine, bali pia unatakiwa uilinde bidhaa kwani bidhaa hupitia misukosuko mingi tangu pale inapozalishwa mpaka inapomfikia mlaji. Pia kila bidhaa ina kifungashio cha aina yake.
Kituo cha Teknolojia ya Ufungashaji (PTC) kina majukumu makuu manne kama ifuatavyo:
- Kusaidia na kuratibu maendeleo ya tasnia ya utungashaji;
- Kutoa mafunzo kwa wazalishaji kuhusiana na teknolojia ya ufungashaji;
- Kudhibiti ubora wa nyenzo za kufungashia ikiwa ni pamoja na kutoa vyeti vya ubora kwa nyezo za kufungashia zilizotengenezwa kwa kuzingatia viwango vya Tanzania;
- Kutoa huduma ya upimaji wa nyenzo za kufungashia.