Ijue Sumukuvu

Sumukuvu (mycotoxin) ni sumu inayozalishwa na kuvu (fungi) ambao wanapatikana kwa asili kwenye mazingira na wanaathiri mazao na kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na mifugo. Sumukuvu huathiri nafaka mfano mahindi, mtama, ngano, uwele na ulezi, karanga, korosho, viungo vilivyokaushwa, mbegu za mafuta(alizeti na pamba) na mazao yatokanayo na mifugo mfano maziwa na mayai.
Uotaji/ukuaji wa kuvu unaweza kutokea kabla au baada ya kuvuna, kipindi cha uhifadhi na kwenye chakula chenyewe hasa kwenye mazingira ya joto, unyevu na machafu. Sumukuvu ni sumu ambazo haziwezi kuondolewa kwa kupikwa au kusindikwa.
Kuna aina mbalimbali za sumukuvu ambazo zimegunduliwa, lakini ambazo zimeonekana kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mifugo ni aflatoxins, ochratoxin A, patulin, fumonisins, zearalenone na nivalenol/deoxynivalenol.
Sumukuvu inapokuwa kwenye chakula ni matokeo ya uchafuzi wa kuvu kwenye mazao kabla na baada ya kuvuna.
Sumukuvu inaweza kumfikia mlaji kwa kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu au kwa kula chakula kitokanancho na mifugo iliyolishwa chakula kilichochafuliwa na sumukuvu mfano maziwa na mayai.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limethibitisha kuwa sumukuvu inaweza kusababisha saratani. Pamoja na hayo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limeweka viwango vinavyovumilika vya sumukuvu kwenye chakula ili kulinda afya ya mlaji.
Nchini Tanzania, nafaka hususan mahindi na karanga ni moja ya vyakula vikuu. Mahindi hutumika kutengeneza chakula cha asili ugali ambacho huliwa karibu kila siku katika familia za Kitanzania. Pia, karanga ni chakula kinachotumika sana maeneo mbalimbali ya nchi kwa mapishi mbalimbali na pia hutumika katika usindikaji wa chakula cha watoto maarafu kama unga lishe. Vyakula hivi viko kwenye hatari zaidi ya kushambuliwa na kuvu ambao wanazalisha sumukuvu. Kwa kuzingatia umuhimu wa nafaka kwa afya ya walaji na kwa kuzingatia uwepo wa makundi maaluma ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa zinazosindikwa kwa kutumia mahindi na karanga, kuna umuhimu mkubwa wakuhakikisha usalama wa mazao haya dhidi ya sumukuvu ili kuwa na taifa lenye afya bora.
Madhara ya kiafya yatokanayo na uchafuzi wa sumukuvu katika chakula
Sumukuvu kama zilivyo sumu zingine husababisha athari za kiafya endapo mlaji atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hiyo. Madhara hayo yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni madhara ambayo hutokea ndani ya muda mrefu na madhara madhara ambayo hutokea ndani ya muda mfupi.
Madhara ya muda mrefu ni yale yanayohusisha kula kiasi kidogo cha chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwa muda mrefu. Mfano wa madhara hayo ni saratini ya figo, ini, tatizo la watoto kuzaliwa na mgongo wazi na damu kutokuganda kwa wakati.
Madhara ya muda mfupi ni yale yanayohusisha kula kiasi kikubwa cha chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwa muda mfupi ambapo ni pamoja na kuharisha, kutapika, maumivu ya tumbo na kuonesha dalili za manjano katika sehemu za mwili mfano kwenye viganja vya mikono, ulim, macho na nyayo.
Nini kifanyike kupunguza au kuondokana na tatizo la uchafuzi w sumukuvu katika chakua
Kupunguza au kuondokana na tatizo la uchafuzi wa sumukuvu ni jukumu la kila mmoja kwenye mnyororo wa thamani wa chakula yaani kuanzia shambani hadi mlaji wa mwisho. Hivyo kila mmoja anatakiwa atomize wajibu wake ili kuwa na chakula salama kwa afya bora.
Hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza athari za sumukuvu nchini kwa kufuata mambo yafuatayo;
- a)Kuhakikisha mahindi na karanga yanakauka vizuri kabla ya kuhifadhi
- b)Kuzingatia kanuni bora za kilimo
- c)Kuzingatia kanuni bora za usindikaji
- d)Uhifadhi sahihi wa malighafi
- e)Uhifadhi sahihi wa bidhaa zilizosindikwa (unga na karanga) majumbani
- f)Kuepuka kulisha wanyama chakula kilichochafuliwa na kuvu
Juhudi za serikali katika kudhibiti uchafuzi wa sumukuvu katika chakula
Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata chakula salama kisichokuwa na sumukuvu imekuwa ikitoa elimu kwa njia mbalimbali, ikiwemo kutumia vyombo vya habari pamoja na kutoa elimu katika maeneo yenye mikusanyika kama vile katika masoko, mikutano ya vijiji, mashule na kliniki za mama na mtoto katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, serikali imeanzisha mradi wa kudhibiti sumukuvu nchini (TANIPAC) chini ya Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), TORDO na VETA.
Mojawapo ya mikakati muhimu ya serikali katika kudhibiti sumukuvu ni kutoa mafunzo kwa wakulima, wasindikaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa mahindi na karanga hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na tatizo la sumukuvu. Hii itasaidia kuboresha mnyororo mzima wa thamani ili kuwa na chakula bora na salama na mwisho kuwa na taifa lenye afya na kukuza uchumi wa nchi.